Al-Mu´taqad as-Swahiyh Shaykh ´Abdus-Salaam Barjas
Yüklə 0.94 Mb.
səhifə7/7
tarix26.04.2016
ölçüsü0.94 Mb.
1   2   3   4   5   6   7

09. ´Aqiydah sahihi juu ya watu wa nyumba ya kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)Katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamoja na kuwapenda watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutambua fadhila na utukufu wao. Katika hali hii mtu anatakiwa kutendea kazi wasia wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Ghaadiyr Khumm. Alimhimidi Allaah na akamsifu, akawaidhisha na kukumbusha. Kisha akasema:

"Amma ba´d: Enyi watu! Hakika mimi si mwingine isipokuwa ni mwanaadamu tu. Anakaribia mjumbe kutoka kwa Mola wangu kunijia [kunichukua] na hapo itabidi niitikie. Nimekuachieni vitu viwili. Cha kwanza ni Kitabu cha Allaah ambacho ndani yake mna uongofu na nuru. Hivyo basi kichukueni Kitabu cha Allaah na shikamaneni nacho."

Akasisitiza juu ya Kitabu cha Allaah halafu akasema:

"Na familia yangu. Ninakukumbusheni juu ya Allaah kwa familia yangu. Ninakukumbusheni juu ya Allaah kwa familia yangu. Ninakukumbusheni juu ya Allaah kwa familia yangu."

Ibn Kathiyr amesema katika Tafsiyr yake:

"Hatuukatai wasia wa watu wa nyumba ya kwa Mtume na kuwatendea wema, kuwaheshimu na kuwatukuza. Hakika wanatokamana na kizazi kisafi na familia tukufu kabisa iliyopo katika uso wa ardhi kifakhari, kiukoo na kinasabu. Hili khasa pale ambapo watakuwa ni wenye kufuata Sunnah ya kinabii, sahihi na ilio wazi. Hali kama hii ndio waliokuwa nayo wahenga wao kama al-´Abbaas na watoto wake na ´Aliy na familia yake na dhuriya yake -Allaah awawie radhi wote."

Miongoni mwa watu wa familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wakeze. Amesema (Ta´ala) kuhusu wao:

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا"Na bakieni majumbani mwenu na wala msionyeshe mapambo uonyeshaji mapambo wa zama za ujahili. Na simamisheni swalah, na toeni zakaah na mtiini Allaah na Mtume Wake. Hakika Allaah Anataka Akuondosheeni uchafu enyi watu wa nyumba na Akutakaseni mtakaso barabara. Na dhukuruni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Ayaat za Allaah na Hikmah, hakika Allaah daima ni Mjuzi, Mwenye khabari." (33:33-34)

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema katika Tafsiyr yake:

"Aayah hii ni dalili juu ya kwamba wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaingia katika familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu wao ndio sababu ya kuteremka kwa Aayah. Sababu ya kuteremka kwa Aayah na kwamba inaingia ndani yake ni jambo lisilokuwa na tofauti juu yake. Ima inaingia na kutumika hiyo tu, jambo ambalo ni maoni moja, au hiyo na nyenginezo, jambo ambalo ndio maoni sahihi zaidi."

al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuoa kwake Zaynab bint Jahsh na humo kumetajwa ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia ndani kwenye chumba cha ´Aaishah na kusema:"Ah-ul-Bayt [watu wa nyumba yangu]! Swalah na salaam iwe juu yao!" Ndipo akasema: "Swalah na salaam iwe juu yako!"

Yaliyotajwa vilevile kuhusiana na fadhila zao, ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ

"Nabii ana haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao na wake zake ni mama zao." (33:06)

Inahusiana na uzito, heshima, maadhimisho, utukufu na wema wa mama wa waumini. Hata hivyo haijuzu kuwa pamoja nao faragha. Ni jambo lenye maafikiano juu ya kwamba nafasi hii haihusiani na wasichana wao na dada zao.


10. ´Aqiydah sahihi juu ya karama za mawaliiAhl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini karama za mawalii ambazo Allaah (Ta´ala) ametaka wafanye, jambo ambalo limetajwa katika Maandiko mengi. Kwa mujibu wao walii ni yule mwenye kutekeleza maamrisho ya Kishari´ah na akajiepusha na yale ambayo yamekatazwa kwa mujibu wa Shari´ah. Amesema (Ta´ala) kuhusu mawalii:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ"Tanabahi!  Hakika vipenzi wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha Allaah." (10:62-63)

 Ili mtu awe sampuli hii ya mtu kunahitajika imani na uchaji Allaah.

Karama ni kitu chenye kwenda kinyume na mazowea ambacho Allaah (Ta´ala) huwafanya wachaji Allaah na waja waumini wakifanye. Mambo hayo yanawasaidia kufanya mambo ya kidini au ya kidunia. Lakini hata hivyo karama za mawalii hazifikii ile daraja ya miujiza ya Manabii na Mitume.

Miongoni mwa karama za mawalii wa Allaah ni kile kisa cha watu wa Pangoni, kisa cha Maryam (Radhiya Allaahu ´anhaa) pindi uchungu ulipompeleka katika shina la mtende ambapo akaamrishwa na Allaah kutikisa mashina yake na matunda yakawa yameanguka pembezoni mwake, kule Allaah kumruzuku kwa njia ya kwamba alikuwa akipata matunda ya majira ya baridi wakati wa joto na matunda ya majira ya joto wakati wa baridi, kisa cha ´Aaswif, ambaye alikuwa ni mwandishi wa Sulaymaan, kisa cha mtu ambaye Allaah alimfisha miaka mia moja halafu baada ya hapo akamuhuisha, kisa cha Jurayj, kisa ch watu watatu katika wana wa Israaiyl ambao walichukua hifadhi kwenye pango na jiwe likawa limeziba maingilio yao na mfano wa visa kama hivyo ambavyo ni vyenye kujulikana kwa wanachuoni na vimethibiti katika Qur-aan, Sunnah iliyothibiti au yaliypokelewa kutoka kwa Salaf au waliokuja baada yao.

Karama itaendelea kuwepo katika Ummah huu hadi Qiyaamah kisimame, kwa kuwa sababu yake ni imani na uchaji Allaah na hivyo vitu viwili vitaendelea kuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.

Lakini ikiwa jambo lenye kwenda kinyume na mazowea linatoka kwa mtu, hiyo haina maana kuwa ni dalili yenye kuonesha wema, imani na uchaji Allaah wake. Katika hali hii ni lazima matendo yake kwanza yalinganishwe na Qur-aan na Sunnah ili kuangalia kama yanaafikiana navyo na kama anavifuata kidhahiri na kindani.


11. ´Aqiydah sahihi juu ya watawala wa waislamuAhl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaitakidi kuwa Allaah (Ta´ala) amewawajibishia waumini kuwatii watawala wao katika yote yasiyokuwa maasi.

Wanaamini maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliyotajwa katika Hadiyth ya ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh):"Sikiliza na utii katika kipindi chako kizito na chepesi, katika unayoyapenda na unayoyachukia hata kama watatawalia juu yako mambo ya kidunia pasi na kukupatia haki yako, hata kama watachukua mali yako na kupiga mgongo wako, midhali haihusiani na maasi."

Wanaonelea kuwa ni haramu kuwafanyia uasi watawala, hata kama watakuwa wakandamizaji na wenye kudhulumu, midhali hawajaona kufuru ya wazi ambayo kwayo wana dalili kutoka kwa Allaah. Hayo ni kutokana na yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):"Wabora wa viongozi wenu ni wale mnaowapenda na wao wanakupendeni na wale mnaowaombea du´aa na wao wanakuombeeni du´aa. Waovu wa viongozi wenu ni wale mnaowachukia na wao wanakuchukieni na mnawalaani na wao wanakulaanini." Kukasemwa: "Ee Mtume wa Allaah! Je, tusipambane nao kwa panga?" Akasema: "Hapana, maadamu wanasimamisha swalah. Mtapoona kitu kutoka kwa watawala wenu mnachokichukia, basi chukieni kitendo chake na wala msinyanyue mkono kutoka katika utiifu."

Katika matamshi mengine imekuja:"Yule aliye na mtawala juu yake na akaona anafanya kitu katika kumuasi Allaah, basi na achukie kitendo kinachomuasi Allaah na wala asinyanyue mkono kutoka katika utiifu." Ameipokea Muslim kutoka kwa ´Awf bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh).

Yule mwenye kutoka katika Mkusanyiko, basi Shari´ah itamuadhibu adhabu kali duniani na Aakhirah kutegemea na ukubwa wa dhambi yake. Mwenye kufa baada ya kutoka katika utiifu na akafarikiana na Mkusanyiko, basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri. Mtu asiulizie juu ya mtu mwenye kufarikiana na Mkusanyiko kutokana na ukubwa wa dhambi yake. Mwenye kufarikiana na Mkusanyiko basi hana hoja yoyote mbele ya Allaah (Ta´ala) siku ya Qiyaamah. Yule mwenye kufarikiana na Mkusanyiko shaytwaan yuko pamoja naye bega kwa bega. Mwenye kufarikiana na Mkusanyiko basi damu yake ni halali.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa ni jambo zuri na lenye kusifika kumuombea mtawala kwa Allaah juu ya mafanikio na usalama. Nayo ni alama yenye kuonesha kuwa mtu ni katika Ahl-us-Sunnah, kama alivyosema Imaam al-Barbahaariy katika kitabu "Sharh-us-Sunnah":

"Ukimuona mtu anaomba dhidi ya mtawala, basi tambue kuwa ni katika watu wenye kufuata matamanio. Na ukimuona mtu anamuombea du´aa mtawala juu ya mafanikio, basi tambua kuwa ni katika watu wa Sunnah - Allaah akitaka."

Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

"Lau mimi ningelikuwa na du´aa [yenye kuitikiwa] basi nisingelimuombea mwengine asiyekuwa mfalme. Tumeamrishwa kuwaombea utengemavu na hatukuamrishwa kuomba dhidi yao hata kama watakuwa ni wakandamizaji na wenye kudhulumu. Ule ukandamizaji na dhuluma zao ni jambo linawapata wao wenyewe na waislamu pia na kutengemaa kwao ni jambo linawapata wao wenyewe na waislamu pia."

Imaam as-Swaabuuniy amesema katika "´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth":

"Wanaonelea kuwaombea utengemavu, mafanikio na uongofu."

Wanaona wale wakubwa wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa ni wenye kuafikiana juu ya kwamba ni haramu kuwatukana. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Wakubwa wetu wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wametukataza [kwa kusema]: "Msiwatukane watawala wenu, msiwafanyie ghushi na wala msiwachukie. Mcheni Allaah na kuweni na subira, hakika mambo yako karibu."" Ameipokea Ibn Abiy ´Aaswim katika "as-Sunnah" na wengineo.


12. Msimamo sahihi juu ya mijadala katika diniAhl-us-Sunnah wal-Jamaa´ahh wanakataza mijadala na mizozo katika dini, kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza hilo.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:"Isomeni Qur-aan maadamu nyoyo zenu zimezunguka kwayo. Mtapotofautiana, basi simameni kutoka kwayo."

Katika "al-Musnad" na "as-Sunan" ya Ibn Maajah - asli matamshi yake yanapatikana katika "as-Swahiyh" ya Muslim kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr - kumesimuliwa:"Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka na wao wakijadiliana juu ya Qadar. Uso wake ukageuka mwekundu kabisa kama mkomamanga. Akasema: "Haya ndio mliyoamrishwa au mliumbwa kwa ajili ya haya? Mnaigonganisha sehemu ya Qur-aan na nyingine. Haya ndio yaliwafanya kuangamia nyumati zilizokuwa kabla yetu.""

Imepokelewa vilevile kuwa mijadala ni njia moja wapo ya adhabu ya Allaah kwa Ummah. Katika "as-Sunan" ya at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kumepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:"Hakuna watu waliopotea baada ya uongofu waliokuwemo isipokuwa baada ya kuanza kujadili." Kisha akasoma:

مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا"Hawakukupigia mfano huo isipokuwa tu kutaka kubisha." (43:58)

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

"Misingi ya Sunnah kwetu ni kushikamana yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwaiga, kuacha Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu, kuacha magomvi na kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´ pamoja na kuacha mizozo, mijadala na magomvi katika dini."

Yote haya yanazingatiwa kuwa ni mijadala ya batili, mijadala ya haki baada ya kuwa haki imeshabainika, mijadala ambayo hoja zake hazitambuliki na yule anayejadiliwa, mijadala juu ya zile Aayah zisizokuwa wazi au mijadala pasi na kuwa na nia nzuri na mfano wa hayo.

Hata hivyo endapo mijadala itakuwa ni yenye kuhusiana na kuidhihirisha na kuibainisha haki na ikawa ni yenye kubainishwa na mwanachuoni aliye na nia nzuri na amelazimiana na adabu, basi inazingatiwa kuwa ni yenye kusifiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ"Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hikmah na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa njia bora zaidi. Hakika Mola wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake Naye Anawajua zaidi walioongoka." (16:125)

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ"Na wala msibishane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni bora zaidi." (29:46)

قَالُوا يَا نُوحُ قَدْ جَادَلْتَنَا فَأَكْثَرْتَ جِدَالَنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ"Wakasema: “Ee Nuuh! Kwa yakini umejadiliana nasi na umekithirisha majadiliano nasi, basi tuletee adhabu unayotutishia nayo ukiwa ni miongoni mwa wakweli."" (11:32)

Kadhalika Amesimulia (Ta´ala) juu ya mjadala wa Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) na watu wake na Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) na Fir´awn. Katika Sunnah kumetajwa mjadala wa Muusa na Aadam (´alayhimaas-Swalaatu was-Salaam) kama ambavyo vilevile kumetajwa mijadala mingi kutoka kwa Salaf. Yote hii ni mijadala yenye kusifiwa midhali ndani yake ina elimu, nia nzuri, yenye kuafikiana na Shari´ah na adabu katika kujadiliana.


13. Matahadharisho ya kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanatahadharisha vikali kabisa kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´ wal-Bid´ah, kwa sababu kukaa nao ni kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah. Isitoshe ni alama ya kuwapenda. Vilevile kunachelea kwa yule mwenye kukaa nao akajisalimisha na upotevu wao na akawafuata katika batili yao. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

"Bid´ah ambayo mtu anazingatiwa kwayo ni katika Ahl-ul-Ahwaa´ ni zile zenye kujulikana kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah zinazoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah. Mfano wa Bid´ah hizo ni kama Bid´ah ya Khawaarij, Raafidhwah, Qadariyyah na Murjia-ah."

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"Na unapowaona wale wanaoziingilia Aayaat Zetu, basi jitenge nao mpaka waingie katika mazungumzo mengineyo. Na kama shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka, usikae pamoja na watu madhalimu." (06:68)

Ibn ´Abbaas amesema:

"Kila mwenye kuzua katika dini ameingia katika Aayah hii na kila mzushi mpaka siku ya Qiyaamah."

Haya yamenukuliwa kutoka kwa al-Baghawiy katika Tafsiyr yake. Ibn Jariyr at-Twabariy amesema:

"Katika Aayah hii kuna dalili ya wazi kabisa juu ya makatazo ya kukaa na watu wa batili kwa sampuli zote za wazushi na watenda madhambi pindi wanapoingilia batili yao."

Ibn ´Abbaas amesema:

"Usiikae na Ahl-ul-Ahwaa´, kwa kuwa kukaa nao kunazigonjwesha nyoyo."

14. Hitimisho ya kitabuMpaka hapa kwa himdi na mafanikio ya Allaah ndio mwisho wa kitabu "al-Mu´taqad as-Swahiyh al-Waajib ´alaa kulli Muslim I´tiqaaduh". Ninamuomba Allaah (Ta´ala) akijaalie kiwe kimefanywa kwa ajili ya Uso Wake Mtukufu, chenye kuafikiana na Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na awanufaishe nacho waislamu wote kwa jumla.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, watu wa nyumbani kwake watwaharifu, Maswahabah zake bora na wale watakaowafuata kwa wema hadi siku ya Malipo.
1 Ahmad na Abu Daawuud kutoka kwa Mu´aawiyah na ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim, adh-Dhahabiy, ash-Shaatwibiy na wengineo. Ahmad, Ibn Maajah na Ibn Abiy ´Aaswim kutoka kwa Anas.

2 Ameipokea al-Aajurriy katika "ash-Shariy´ah" kutoka ´Abdullaah bin ´Amr na at-Twabaraaniy katika "as-Swaghiyrah" na katika "al-Awsatw" kutoka kwa Anas bin Maalik.

3 Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah.

4 Tazama ”Silsilah al-Ahaadiyth as-Sahiyhah” (6/358/2668) ya Imam Muhammad Naaswir-ud-Dîn al-Albaaniy.

5an-Nubuwwaat” ya Shaykh-ul-Islaam, uk. 255.

www.firqatunnajia.com


1   2   3   4   5   6   7


Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©azrefs.org 2016
rəhbərliyinə müraciət

    Ana səhifə